10 Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi?
11 Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha za wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao;
12 basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.
13 Akaja Sulemani kutoka mahali pa juu pa Gibeoni, toka mbele ya hema ya kukutania, mpaka Yerusalemu; akatawala juu ya Israeli.
14 Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu na mia nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.
15 Mfalme akafanya fedha na dhahabu kuwa kama mawe humo Yerusalemu, na mierezi akaifanya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi.
16 Nao farasi, aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi; kila kundi na thamani yake.