11 Amazia akapiga moyo konde, akawaongoza watu wake, akaenda mpaka Bonde la Chumvi, akawapiga katika wana wa Seiri watu elfu kumi.
12 Na elfu kumi wengine, ambao wana wa Yuda waliwachukua wali hai, wakawaleta juu ya jabali, wakawaangusha toka juu ya jabali, hata wakavunjika-vunjika wote.
13 Lakini wale watu wa jeshi, aliowarudisha Amazia, wasiende naye vitani, hao wakaiteka miji ya Yuda, tangu Samaria mpaka Beth-horoni, wakawapiga watu elfu tatu, wakachukua nyara nyingi.
14 Basi ikawa, Amazia alipokwisha rudi kutoka kuwaua Waedomi, alileta miungu ya wana wa Seiri, akaisimamisha kuwa miungu yake, akajiinama mbele yao, akaifukizia uvumba.
15 Kwa hiyo hasira ya BWANA ikawaka juu ya Amazia, akampelekea nabii, aliyemwambia, Mbona umeitafuta miungu ya watu, isiyowaokoa watu wao mkononi mwako?
16 Ikawa, aliposema naye, mfalme akamwambia, Je! Tumekutia wewe kuwa mshauri wa mfalme? Nyamaza; kwa nini upigwe? Ndipo yule nabii akaacha, akasema, Najua ya kuwa Mungu amekusudia kukuangamiza, kwa sababu umeyafanya haya, wala hukulisikiliza shauri langu.
17 Ndipo mfalme Amazia akafanya shauri, akatuma wajumbe kwa Yehoashi, mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, kusema, Njoo, tutazamane uso kwa uso.