7 Akazibomoa madhabahu, akaponda-ponda maashera na sanamu kuwa mavumbi, akazikata-kata sanamu zote za jua katika nchi yote ya Israeli, kisha akarejea Yerusalemu.
8 Hata katika mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwake, alipokwisha kuisafisha nchi, na nyumba, akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, na Maaseya, akida wa mji, na Yoa, mwana wa Yoahazi, mwandishi wa tarehe, waitengeneze nyumba ya BWANA, Mungu wake.
9 Wakamjia Hilkia kuhani mkuu, wakampa fedha, iliyoletwa nyumbani mwa Mungu, waliyoikusanya Walawi, wangoje mlango, mikononi mwa Manase na Efraimu, na mabaki yote ya Israeli, na Yuda yote na Benyamini, na wenyeji wa Yerusalemu.
10 Wakaitia mikononi mwa watenda kazi walioisimamia nyumba ya BWANA; na hao mafundi waliotenda kazi nyumbani mwa BWANA wakaitoa kwa kuitengeneza na kuifanya upya nyumba;
11 wakawapa maseremala na waashi, ili wanunue mawe ya kuchonga, na miti ya kuungia, na kuifanyiza boriti kwa nyumba zile walizoziharibu wafalme wa Yuda.
12 Nao watu wakatenda kazi kwa uaminifu; na wasimamizi wao walikuwa Yahathi na Obadia, Walawi, wa wana wa Merari; na Zekaria na Meshulamu, wa wana wa Wakohathi, ili kuihimiza kazi; na wengine katika Walawi, wote waliokuwa wastadi wa kupiga vinanda.
13 Tena walikuwa juu ya wachukuzi wa mizigo, wakawahimiza wote waliotenda kazi ya huduma yo yote; na miongoni mwa Walawi kulikuwa na waandishi, na wasimamizi, na mabawabu.