8 Basi, wakati ule Sulemani akafanya sikukuu, na Israeli wote pamoja naye, kusanyiko kubwa sana, toka maingilio ya Hamathi mpaka kijito cha Misri, muda wa siku saba.
9 Hata siku ya nane wakaita kusanyiko la makini; kwa maana walishika kuitakasa madhabahu siku saba, na sikukuu siku saba.
10 Akawaruhusu watu waende hemani kwao siku ya ishirini na tatu, ya mwezi wa saba, wakifurahi na kuchangamka mioyoni kwa wema wote BWANA aliomfanyia Daudi, na Sulemani, na Israeli watu wake.
11 Hivyo Sulemani akaimaliza nyumba ya BWANA, na nyumba ya mfalme; na yote yaliyomwingia Sulemani moyoni ayafanye nyumbani mwa BWANA, na nyumbani mwake mwenyewe, akayafanikisha.
12 BWANA akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu.
13 Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni;
14 ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.