1 Ndipo Sofari Mnaamathi akajibu, na kusema,
2 Je! Huu wingi wa maneno usijibiwe?Na mtu aliyejaa maneno, je! Ahesabiwe kuwa na haki?
3 Je! Majivuno yako yawanyamazishe watu wawe kimya?Nawe hapo ufanyapo dhihaka, je! Hapana mtu atakayekutahayarisha?
4 Kwa kuwa wewe wasema, Mafunzo yangu ni safi,Nami ni safi machoni pako.
5 Lakini, laiti Mungu angenena,Na kuifunua midomo yake juu yako;
6 Tena akuonyeshe hizo siri za hekima,Ya kuwa hufanikiwa katika kuyatimiza makusudi yake!Ujue basi ya kuwa Mungu akuachilia katika uovu wako.
7 Je! Wewe waweza kuuvumbua ukuu wa Mungu?Waweza kuufikilia upeo wa huyo Mwenyezi?
8 Ni juu mno kama mbingu; waweza kufanya nini wewe?Ni wenye kina kuliko kuzimuni; waweza kujua nini wewe?
9 Cheo chake ni kirefu kuliko dunia,Ni kipana zaidi ya bahari.
10 Yeye akipita, na kufunga watu,Na kuwaita hukumuni, ni nani basi awezaye kumzuia?
11 Kwani yeye awajua watu baradhuli;Huona na uovu pia, hata asipoufikiri.
12 Lakini mpumbavu aweza kupata ufahamu,Ingawa mwanadamu huzaliwa kama mtoto wa punda-mwitu.
13 Wewe ukiuweka moyo wako kwa uelekevu,Na kumnyoshea mikono yako;
14 Ikiwa una uovu mkononi mwako, uweke mbali nawe,Wala usikubali upuzi kukaa hemani mwako;
15 Hakika ndipo utakapopata kuinua uso pasipo ila;Naam, utathibitika, wala hutakuwa na hofu;
16 Kwa kuwa utasahau mashaka yako;Utayakumbuka kama maji yaliyokwisha pita;
17 Na maisha yako yatakuwa meupe kuliko adhuhuri;Lijapokuwa ni giza, litakuwa kama alfajiri.
18 Nawe utakuwa salama, kwa sababu kuna matumaini;Naam, utatafuta-tafuta kando yako, na kupumzika katika salama.
19 Tena utalala, wala hapana atakayekutia hofu;Naam, wengi watakutafuta uso wako.
20 Lakini macho ya waovu yataingia kiwi,Nao hawatakuwa na njia ya kukimbilia,Na matumaini yao yatakuwa ni kutoa roho.