1 Mbona nyakati zisiwekwe na Mwenyezi?Na hao wamjuao mbona hawazioni siku zake?
2 Wako waziondoao alama za mipaka;Huyachukua makundi kwa jeuri na kuyalisha.
3 Humfukuza punda wake asiye baba,Humtwaa rehani ng’ombe wake mwanamke mjane.
4 Humgeuza mhitaji aiache njia;Maskini wa nchi hujificha pamoja.
5 Tazama, kama punda-mwitu jangwaniWao hutoka kwenda kazini mwao, wakitafuta chakula kwa bidii;Jangwa huwapa chakula cha watoto wao.
6 Hukata nafaka zao mashambani;Na kuokota zabibu za waovu.
7 Hujilaza usiku kucha uchi pasipo nguo,Wala hawana cha kujifunika baridi.
8 Hutota kwa manyunyo ya milimani,Na kuambatana na jabali kwa kukosa sitara,
9 Wako wamwondoao matitini kwa nguvu huyo asiye na baba,Na kutwaa rehani kwa maskini;
10 Hata wazunguke uchi pasipo mavazi,Nao wakiwa na njaa huchukua miganda;
11 Hushindika mafuta ndani ya makuta ya watu hao;Wakanyaga mashinikizo, nao wana kiu.
12 Watu huugua toka mji ulio na watu wengi,Na roho yake aliyejeruhiwa hupiga ukelele;Wala Mungu hauangalii upumbavu.
13 Hawa ni katika hao waliouasi mwanga;Hawazijui njia zake,Wala hawakai katika mapito yake.
14 Mwuaji huamka asubuhi kukipambauka, huwaua maskini na wahitaji;Tena wakati wa usiku yu kama mwivi.
15 Tena jicho lake mzinifu hungojea wakati wa giza-giza,Akisema, Hapana jicho litakaloniona;Naye huuficha uso wake.
16 Wao hutoboa nyumba gizani;Hujifungia ndani wakati wa mchana;Hawaujui mwanga.
17 Kwani asubuhi kwao wote ni kama giza tupu;Kwani wao wavijua vitisho vya hiyo giza tupu.
18 Mwasema, Yeye ni mwepesi juu ya uso wa gharika;Sehemu yao inalaaniwa duniani;Hageuki kwenda njia ya mizabibuni.
19 Chaka na hari hukausha maji ya theluji;Kuzimu nako hao ambao wamefanya dhambi.
20 Tumbo lililomzaa litamsahau; buu litamla na kuona tamu;Hatakumbukwa tena;Na udhalimu utavunjwa kama mti.
21 Naam, yeye huwala walio tasa wasiozaa;Wala hamtendei mema mwanamke mjane.
22 Lakini Mungu huwadumisha wenye uwezo kwa nguvu zake;Huinuka, wasiokuwa na tumaini la kuishi.
23 Huwapa kuwa na salama, nao wapumzika kwayo;Na macho yake ya juu ya njia zao.
24 Wao wametukuzwa; lakini kitambo kidogo hutoweka;Naam, hushushwa, na kuondolewa njiani kama wengine wote,Nao hukatwa kama vile masuke ya ngano.
25 Na kama sivyo sasa, ni nani atakayenihukumu kuwa ni mwongo,Na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?