1 Tazama, jicho langu limeyaona hayo yote,Sikio langu limeyasikia na kuelewa nayo.
2 Hayo myajuayo ninyi, na mimi pia nayajua;Mimi si duni kuliko ninyi.
3 Hakika ningenena naye huyo Mwenyezi,Nami nataka kuhojiana na Mungu.
4 Lakini ninyi hubuni maneno ya uongo,Ninyi nyote ni matabibu wasiofaa.
5 Laiti mngenyamaza kabisa!Hilo lingekuwa hekima kwenu.
6 Sikieni sasa basi hoja zangu,Mkayasikie mashindano ya midomo yangu.
7 Je! Mtanena yasiyo ya haki kwa ajili ya Mungu,Na kusema kwa udanganyifu kwa ajili yake?
8 Je! Mtamwonyesha yeye upendeleo?Mtamtetea Mungu?
9 Je! Itafaa yeye kuwatafuta ninyi?Au, kama kumdanganya mtu, je! Mtamdanganya yeye?
10 Hakika atawakemea ninyi,Mkiwapendelea watu kwa siri.
11 Je! Huo ukuu wake hautawatia hofu,Na utisho wake hautawaangukia?
12 Matamko yenu ya hekima ni mithali ya majivu,Ngome zenu ni ngome za udongo.
13 Nyamazeni, niacheni, ili nipate kunena,Na hayo yatakayonijilia na yaje.
14 Nitaitwaa nyama ya mwili wangu katika meno yangu,Na kuutwaa uhai wangu mkononi mwangu!
15 Tazama, ataniua; sina tumaini;Ila hata hivyo nitaithibitisha njia yangu mbele yake.
16 Hili nalo litakuwa ni wokovu wangu;Kwani asiyemcha Mungu hatakaribia mbele yake.
17 Sikieni sana maneno yangu,Maelezo yangu na yaingie masikioni mwenu.
18 Angalieni sasa, nimekwisha kulitengeneza neno langu,Najua ya kuwa ni mwenye haki mimi.
19 Yuko nani atakayeshindana nami?Maana sasa nitanyamaa kimya na kutoa roho.
20 Lakini msinifanyie mambo mawili, hayo tu,Ndipo nami sitajificha usoni pako;
21 Uondoe mkono wako usinilemee;Na utisho wako usinitie hofu.
22 Basi uite wakati huo, nami nitaitika;Au, niache ninene mimi, nawe unijibu.
23 Maovu yangu na dhambi zangu ni ngapi?Nijulishe kosa langu na dhambi yangu.
24 Mbona umeuficha uso wako,Na kunihesabu kuwa ni adui yako?
25 Je! Utalitaabisha jani lipeperushwalo?Au, je! Utayafuatia hayo mabua makavu?
26 Kwani umeandika maneno ya uchungu juu yangu,Na kunirithisha maovu ya ujana wangu;
27 Waitia miguu yangu katika mkatale, na kuyaaua mapito yangu yote;Wajiandikia alama kuzizunguka nyayo za miguu yangu;
28 Nijapokuwa ni kama kitu kilichooza, kinachosinyaa,Mfano wa nguo iliyoliwa na nondo.