1 Ndipo Ayubu akajibu, na kusema,
2 Hata leo mashitaka yangu yana uchungu;Pigo langu ni zito zaidi ya kuugua kwangu.
3 Laiti ningejua mahali niwezapo kumwona,Nifike hata hapo anapokaa!
4 Ningeiweka daawa yangu mbele yake,Na kukijaza kinywa changu hoja.
5 Ningeyajua maneno atakayonijibu,Na kuelewa na hayo atakayoniambia.
6 Je! Angeshindana nami kwa ukuu wa uwezo wake?La, lakini angenisikiliza.
7 Hapo walekevu wangepata kuhojiana naye;Basi hivyo ningeachiliwa na mwamuzi wangu milele.
8 Tazama, naenda mbele, wala hayuko;Narudi nyuma, lakini siwezi kumwona;
9 Na mkono wa kushoto, afanyapo kazi, lakini siwezi kumwona;Hujificha upande wa kuume, hata nisimwone.
10 Lakini yeye aijua njia niendeayo;Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.
11 Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake;Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka.
12 Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake;Nimeyatunza maneno ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,
13 Lakini yeye ni mmoja, ni nani awezaye kumgeuza?Tena nafsi yake ilitakalo, ndilo afanyalo.
14 Kwani yeye hulitimiliza hilo nililoamuriwa;Tena mambo mengi kama hayo ya pamoja naye.
15 Kwa hiyo naona taabu mbele ya uso wake;Nitakapofikiri, namwogopa.
16 Kwani Mungu ameufanya moyo wangu kuzimia,Naye Mwenyezi amenitaabisha;
17 Maana sikufadhaishwa kwa sababu ya giza,Wala kwa sababu giza kuu limenifunika uso.