Ayu.

Sura 29

Swahili Union Version

Ayubu Amalizia Hoja Zake

1Kisha Ayubu akaendelea na mithali yake, na kusema, 2Laiti ningekuwa kama nilivyokuwa katika miezi ya kale,Kama katika siku hizo Mungu aliponilinda; 3 Hapo taa yake ilipomulika juu yangu kichwani,Nami nilitembea gizani kwa njia ya mwanga wake; 4 Kama nilivyokuwa katika siku zangu za kukomaa,Hapo siri ya Mungu ilipokuwa hemani mwangu; 5Wakati Mwenyezi alipokuwa akali pamoja nami,Nao watoto wangu walipokuwa wakinizunguka; 6 Wakati hatua zangu zilipokuwa zikioshwa kwa siagi,Nalo jabali liliponimiminia mito ya mafuta! 7Wakati nilipotoka kwenda mjini, hata langoni,Nilipokitengeza kiti changu katika njia kuu, 8Hao vijana waliniona wakajificha,Nao wazee wakaniondokea na kusimama; 9Wakuu wakanyamaa wasinene,Na kuweka mikono yao vinywani mwao; 10 Sauti yao masheki ilinyamaa,Na ndimi zao zilishikamana na makaakaa yao. 11Maana sikio liliponisikia, ndipo likanibarikia;Na jicho liliponiona, likanishuhudia. 12 Kwa sababu nalimwokoa maskini aliyenililia;Yatima naye, na yule asiyekuwa na mtu wa kumsaidia. 13Baraka yake yeye aliyekuwa karibu na kupotea ilinijia;Nikaufanya moyo wa mjane kuimba kwa furaha. 14 Nalijivika haki, ikanifunika,Adili yangu ilikuwa kama joho na kilemba. 15 Nalikuwa macho kwa kipofu,Nalikuwa miguu kwa aliyechechemea. 16 Nalikuwa baba kwa mhitaji,Na daawa ya mtu nisiyemjua naliichunguza. 17Nami nilizivunja taya za wasio haki,Na kumpokonya mawindo katika meno yake. 18 Ndipo niliposema, Nitakufa ndani ya kioto changu,Nami nitaziongeza siku zangu kama mchanga; 19 Shina langu limeenea hata kufika majini,Na umande hukaa usiku kucha katika matawi yangu; 20 Utukufu wangu utakuwa mpya kwangu,Na uta wangu hurejezwa upya mkononi mwangu. 21Watu walitega masikio kunisikiliza, na kungoja,Wakanyamaa kimya wapate sikia mashauri yangu. 22Hawakunena tena baada ya kusikia maneno yangu;Matamko yangu yakadondoka juu yao. 23Walikuwa wakiningojea kama kungojea mvua;Wakafunua vinywa vyao sana kama mvua ya masika. 24Walipokata tamaa nikacheka nao;Na mwanga wa uso wangu hawakuuangusha. 25Niliwachagulia njia, nikakaa kama mkuu wao.Nikakaa kama mfalme katika jeshi la askari,Mfano wa awafarijiye hao waombolezao.