Hab. 1 SUV

Lalamiko la Nabii

1 Ufunuo aliouona nabii Habakuki.

2 Ee BWANA, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa.

3 Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea.

4 Kwa sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka.

5 Angalieni, enyi mlio kati ya mataifa, katazameni, kastaajabuni sana; kwa maana mimi natenda tendo siku zenu, ambalo hamtaliamini hata mkiambiwa.

6 Kwa maana, angalieni, nawaondokesha Wakaldayo, taifa lile kali, lenye haraka kupita kiasi; wapitao katikati ya dunia, ili wayamiliki makao yasiyo yao.

7 Hao ni watu wa kutisha sana, wa kuogofya sana; hukumu yao na ukuu wao hutoka katika nafsi zao wenyewe.

8 Farasi zao ni wepesi kuliko chui, ni wakali kuliko mbwa-mwitu wa jioni; na wapanda farasi wao hujitapa naam, wapanda farasi wao watoka mbali sana; huruka kama tai afanyaye haraka ale.

9 Waja wote ili kufanya udhalimu; nyuso zao zimeelekezwa kwa bidii yao kama upepo wa mashariki, nao hukusanya mateka kama mchanga.

10 Naam, huwadhihaki wafalme, na wakuu ni kitu cha kudharauliwa kwake; huidharau kila ngome; kwa maana hufanya chungu ya mavumbi, na kuitwaa.

11 Kisha atapita kwa kasi, kama upepo, atapita na kuwa ana hatia; yeye ambaye nguvu zake ni mungu wake.

12 Ee BWANA, Mungu wangu, mtakatifu wangu, wewe si wa milele? Hatutakufa. Ee BWANA, umemwandikia hukumu, nawe, Ee Jabali, umemweka imara ili aadhibishwe.

13 Wewe uliye na macho safi hata usiweze kuangalia uovu, wewe usiyeweza kutazama ukaidi, mbona unawaangalia watendao kwa hila; na kunyamaza kimya, hapo mtu mwovu ammezapo mtu aliye mwenye haki kuliko yeye;

14 na kufanya wanadamu kuwa kama samaki wa baharini, kama vitu vitambaavyo, ambavyo havina mtawala?

15 Yeye huwatoa wote kwa ndoana yake, huwakamata katika wavu wake, na kuwakusanya katika juya lake; ndiyo sababu afurahi na kupendezwa.

16 Kwa sababu hiyo huutolea wavu wake sadaka, na kulifukizia uvumba juya lake; kwa sababu kwa vitu vile fungu lake limenona, na chakula chake kimekuwa tele.

17 Je! Atawatoa walio katika wavu wake, asiache kuwaua watu wa mataifa daima?

Sura

1 2 3