Hab. 3 SUV

Ombi la Nabii

1 Sala ya nabii Habakuki.

2 Ee BWANA, nimesikia habari zako, nami naogopa;Ee BWANA, fufua kazi yako katikati ya miaka;Katikati ya miaka tangaza habari yake;Katika ghadhabu kumbuka rehema.

3 Mungu alikuja kutoka Temani,Yeye aliye mtakatifu kutoka mlima Parani.Utukufu wake ukazifunika mbingu,Nayo dunia ikajaa sifa yake.

4 Mwangaza wake ulikuwa kama nuru;Alikuwa na mishale ya nuru ubavuni pake;Ndipo ulipofichwa uweza wake.

5 Mbele zake ilikwenda tauni,Na makaa ya moto yakatoka miguuni pake.

6 Akasimama, akaitetemesha dunia;Akatazama, akawasitusha mataifa;Na milima ya zamani ikatawanyika;Vilima vya kale vikainama;Miendo yake ilikuwa kama siku za kale.

7 Naliziona hema za Kushani katika taabu;Mapazia ya nchi ya Midiani yakatetemeka.

8 Je! BWANA aliikasirikia mito?Je! Hasira yako ilikuwa juu ya mito,Au ghadhabu yako juu ya bahari,Hata ukapanda farasi zako,Katika magari yako ya wokovu?

9 Uta wako ukafanywa wazi kabisa;Viapo walivyopewa kabila vilikuwa neno thabiti;Ukaipasua nchi kwa mito.

10 Milima ilikuona, ikaogopa;Gharika ya maji ikapita;Vilindi vikatoa sauti yake,Vikainua juu mikono yake.

11 Jua na mwezi vikasimama makaoni mwao;Mbele ya nuru ya mishale yako ilipotapakaa,Mbele ya mwangaza wa mkuki wako umeremetao.

12 Ulikwenda katikati ya nchi kwa ghadhabu;Ukawapura mataifa kwa hasira.

13 Ukatokea kwa ajili ya wokovu wa watu wako,Kwa ajili ya wokovu wa masihi wako;Ukakiponda kichwa cha nyumba ya waovu,Ukiuweka wazi msingi hata mwambani.

14 Ukakichoma kichwa cha mashujaa wake kwa fimbo zao wenyewe;Wakaja kama kisulisuli ili kunitawanya;Kama wakifurahi kuwameza maskini kwa siri.

15 Ukaikanyaga bahari kwa farasi zako,Chungu ya maji yenye nguvu.

16 Nikasikia, na tumbo langu likatetemeka,Midomo yangu ikatikisika kwa sauti ile;Ubovu ukaingia mifupani mwangu,Nikatetemeka katika mahali pangu;Ili nipate kuingoja ile siku ya dhiki,Kundi lao washambuliao wakweapo juu ya watu.

Imani na Shangwe katika Shida

17 Maana mtini hautachanua maua,Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda;Taabu ya mzeituni itakuwa bure,Na mashamba hayatatoa chakula;Zizini hamtakuwa na kundi,Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng’ombe;

18 Walakini nitamfurahia BWANANitamshangilia Mungu wa wokovu wangu.

19 YEHOVA, aliye BWANA, ni nguvu zangu,Yeye huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu,Naye ataniendesha katika mahali pangu palipoinuka.

Sura

1 2 3