1 Na Mkanaani, mfalme wa Aradi, aliyeketi upande wa Negebu, alisikia habari ya kuwa Israeli alikuja kwa njia ya Atharimu; basi akapigana na Israeli, na watu kadha wa kadha miongoni mwao akawateka mateka.
2 Basi Israeli akaweka nadhiri kwa BWANA akasema, Kama wewe utawatia watu hawa mikononi mwangu kweli ndipo mimi nitaiharibu miji yao kabisa.
3 BWANA akasikiza sauti ya Israeli, akawatia Wakanaani mikononi mwao; nao wakawaharibu wao na miji yao kabisa; na jina la mahali hapo likaitwa Horma.
4 Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia.
5 Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.
6 BWANA akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.
7 Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa BWANA, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu.