1 Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya BWANA.
2 Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wamejivika nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi.
3 Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa.
4 Yamkini BWANA, Mungu wako, atayasikia maneno ya huyo amiri ambaye mfalme wa Ashuru, bwana wake, amemtuma ili amtukane Mungu aliye hai; na BWANA, Mungu wako atayakemea maneno aliyoyasikia; basi, inua dua yako kwa ajili ya mabaki yaliyobakia.
5 Basi, watumishi wa mfalme Hezekia wakaenda kwa Isaya.