14 BWANA asema hivi, Kazi ya Misri, na bidhaa ya Kushi, na Waseba, watu walio warefu, watakujilia, nao watakuwa wako; watakufuata; watakuja katika minyororo; wataanguka chini mbele yako, watakuomba, wakisema, Hakika Mungu yu ndani yako; wala hapana mwingine, hapana Mungu tena.
15 Hakika wewe u Mungu ujifichaye nafsi yako, Ee Mungu wa Israeli, Mwokozi.
16 Watatahayarika, naam, watafadhaika, wote pia; wale wafanyao sanamu wataingia fadhaa pamoja.
17 Bali Israeli wataokolewa na BWANA kwa wokovu wa milele; ninyi hamtatahayarika, wala kufadhaika, milele na milele.
18 Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine.
19 Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi, BWANA, nasema haki; nanena mambo ya adili.
20 Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi wa mataifa mliookoka; hawana maarifa wale wachukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga; wamwombao mungu asiyeweza kuokoa.