3 Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu.
4 Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu?
5 Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa;
6 nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.
7 Kwa maana shamba la mizabibu la BWANA wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio.
8 Ole wao waongezao nyumba baada ya nyumba, na kuweka shamba karibu na shamba, hata hapana nafasi tena, nanyi hamna budi kukaa peke yenu kati ya nchi!
9 BWANA wa majeshi asema katika masikio yangu, Hakika majumba mengi yatakuwa ukiwa, naam, majumba makubwa, mazuri, yatakuwa hayana watu.