3 Kwa maana utaenea upande wa kuume na upande wa kushoto; na wazao wako watawamiliki mataifa; wataifanya miji iliyokuwa ukiwa kukaliwa na watu.
4 Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena.
5 Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote.
6 Maana BWANA amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako.
7 Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya.
8 Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema BWANA, Mkombozi wako.
9 Kwa maana jambo hili limekuwa kama maji ya Nuhu kwangu; maana kama nilivyoapa ya kwamba maji ya Nuhu hayatapita juu ya dunia tena, kadhalika nimeapa ya kwamba sitakuonea hasira, wala kukukemea.