11 nawe utafurahi mbele ya BWANA, Mungu wako, wewe na mwana wako na binti yako, na mtumwa wako na mjakazi wako, na Mlawi aliye ndani ya malango yako, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio katikati yako, katika mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake.
12 Nawe kumbuka kwamba ulikuwa mtumwa huko Misri; tena zishike amri hizi kwa kuzifanya.
13 Fanya sikukuu ya vibanda siku saba, utakapokwisha kuyakusanya yatokayo katika sakafu yako ya nafaka, na katika kinu chako cha divai;
14 nawe utafurahi katika sikukuu yako, wewe, na mwanao, na binti yako, na mtumwa wako, na mjakazi wako, na Mlawi, na mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe, walio ndani ya malango yako.
15 Siku saba mfanyie sikukuu BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua BWANA; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, atakubarikia katika maongeo yako yote, na katika kazi zote za mikono yako, nawe uwe katika kufurahi kabisa.
16 Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele za BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala wasitokee mbele za BWANA mikono mitupu.
17 Kila mtu na atoe kama awezavyo, kwa kadiri ya baraka ya BWANA, Mungu wako, alivyokupa.