15 Na Makiri nilimpa Gileadi.
16 Na Wareubeni na Wagadi niliwapa tokea Gileadi mpaka bonde la Arnoni, katikati ya bonde, na mpaka wake; mpaka mto wa Yaboki, nao ni mpaka wa wana wa Amoni;
17 na nchi ya Araba nayo, na mto wa Yordani, na mpaka wake, tokea Kinerethi mpaka bahari ya hiyo Araba, nayo ni Bahari ya Chumvi, chini ya matelemko ya Pisga, upande wa mashariki.
18 Nikawaamuru wakati huo, nikawaambia, BWANA, Mungu wenu, amewapa ninyi nchi hii mwimiliki, basi vukeni ng’ambo wenye silaha mbele ya ndugu zenu, wana wa Israeli, nyote mlio mashujaa.
19 Lakini wake wenu na watoto wenu, na wanyama wenu wa mji, (nawajua kwamba mna wanyama wengi), na wakae katika miji yenu niliyowapa;
20 hata BWANA awapumzishe ndugu zenu kama ninyi, nao pia waimiliki nchi wapewayo na BWANA, Mungu wenu, ng’ambo ya Yordani; ndipo mtakaporudi kila mmoja aende katika milki yake niliyowapa.
21 Nikamwamuru Yoshua wakati huo, nikamwambia, Macho yako yameona yote aliyowatenda BWANA, Mungu wenu, wale wafalme wawili, navyo ndivyo atakavyoutenda BWANA kila ufalme huko uvukiako.