26 kisha katika kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichokuwa pale mbele za BWANA, akatwaa mkate mmoja usiochachwa, na mkate mmoja ulioandaliwa na mafuta na kaki moja nyembamba, akaiweka juu ya mafuta, na juu ya huo mguu wa nyuma wa upande wa kuume;
27 kisha akaweka vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe, na kuvitikisa huku na huku viwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA.
28 Kisha Musa akavitwaa tena mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa vilikuwa vya kuwaweka wakfu, ni harufu nzuri; ilikuwa dhabihu iliyosongezwa kwa BWANA kwa moto.
29 Kisha Musa akakitwaa kile kidari, akakitikisa huku na huku, kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za BWANA; ni sehemu ya Musa katika huyo kondoo mume wa kuwaweka wakfu; kama BWANA alivyomwagiza Musa.
30 Kisha Musa akatwaa baadhi ya mafuta ya kutia, na ya damu iliyokuwa pale juu ya madhabahu, na kumnyunyizia Haruni, katika mavazi yake, na wanawe, katika mavazi yao, pamoja naye; akamtakasa Haruni, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye.
31 Kisha Musa akawaambia huyo Haruni na wanawe, Tokoseni hiyo nyama mlangoni pa hema ya kukutania; mkaile pale pale, na hiyo mikate iliyo katika kile kikapu cha kuwaweka wakfu, kama nilivyoagizwa kusema, Haruni na wanawe wataila.
32 Nacho kitakachosalia katika hiyo nyama na mikate mtakichoma moto.