11 Ndipo utakapowaambia, Ni kwa sababu baba zenu wameniacha mimi, asema BWANA, na kuwafuata miungu mingine, na kuwatumikia, na kuwaabudu, wakaniacha mimi, wasiishike torati yangu;
12 na ninyi mmetenda mabaya kupita baba zenu; maana angalieni, mnaenenda kila mmoja wenu kwa ushupavu wa moyo wake mbaya, msinisikilize mimi;
13 basi, kwa sababu hiyo, nitawatoeni katika nchi hii, na kuwaingiza katika nchi ambayo hamkuijua, wala ninyi wala baba zenu; na huko mtawatumikia miungu mingine mchana na usiku; kwa maana mimi sitawapa fadhili zangu hata kidogo.
14 Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema BWANA, ambapo hawatasema tena, Aishivyo BWANA, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya Misri;
15 lakini, Aishivyo BWANA, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya kaskazini, na toka nchi zote alikowafukuza; nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe niliyowapa baba zao.
16 Tazama, asema BWANA, Nitatuma watu kuwaita wavuvi wengi, nao watawavua; na baada ya hayo nitatuma watu kuwaita wawindaji wengi, nao watawawinda, watoke katika kila mlima, na kila kilima, na pango za majabali.
17 Maana macho yangu yaziangalia njia zao zote, hawakufichwa uso wangu usiwaone, wala haukusitirika uovu wao macho yangu yasiuone.