16 Hata nikiisha kumpa Baruku, mwana wa Neria, hati ile ya kununua, nalimwomba BWANA, nikisema,
17 Aa! Bwana MUNGU, tazama, wewe umeziumba mbingu na nchi, kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyoshwa; hapana neno lililo gumu usiloliweza;
18 wewe uwarehemuye watu elfu nyingi, uwalipaye baba za watu uovu wao vifuani mwa watoto wao baada yao; Mungu aliye mkuu, aliye hodari, BWANA wa majeshi ndilo jina lake;
19 mkuu wa mashauri, mweza katika kutenda; ambaye macho yake yamefumbuka juu ya njia zote za wanadamu, kumpa kila mtu kwa kadiri ya njia zake, na kwa kadiri ya matunda ya matendo yake,
20 wewe uliyeweka ishara na ajabu katika nchi ya Misri hata siku hii ya leo, katika Israeli na kati ya watu wengine; na kujifanyia jina kama ilivyo leo;
21 ukawatoa watu wako, Israeli, katika nchi ya Misri, kwa ishara, na kwa ajabu, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mkuu;
22 ukawapa nchi hii, uliyowaapia baba zao kwamba utawapa, nchi iliyojaa maziwa na asali;