23 nao wakaingia, wakaimiliki; lakini hawakuitii sauti yako, wala hawakuenda katika sheria yako; hawakutenda neno lo lote katika haya uliyowaagiza wayatende; basi, kwa sababu hii umeleta juu yao mabaya haya yote;
24 angalia maboma haya; wameujia mji huu ili kuutwaa; na mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo wanaopigana nao, kwa sababu ya upanga, na njaa, na tauni; na hayo uliyosema yamekuwa; na, tazama, wewe unayaona.
25 Nawe, Ee Bwana MUNGU, umeniambia, Jinunulie shamba lile kwa fedha, ukawaite mashahidi; iwapo mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo; je! Itakuwaje?
26 Ndipo neno la BWANA likamjia Yeremia, kusema,
27 Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?
28 Basi, BWANA asema hivi, Tazama, nitautia mji huu katika mikono ya Wakaldayo, na katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, naye atautwaa;
29 na Wakaldayo, wanaopigana na mji huu, watakuja, na kuutia moto mji huu, na kuuteketeza, pamoja na nyumba zake, ambazo juu ya dari zake wamemfukizia Baali uvumba, na kuwamiminia miungu mingine vinywaji, ili kunikasirisha.