13 BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalifanya agano na baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa, nikisema,
14 Mwisho wa kila mwaka wa saba kila mtu na amweke huru ndugu yake aliye Mwebrania, aliyeuzwa kwako na kukutumikia miaka sita utamwacha atoke kwako huru, lakini baba zenu hawakunisikiliza, wala hawakutega masikio yao.
15 Na ninyi mlikuwa mmegeuka, mkafanya yaliyo haki machoni pangu, kwa kumtangazia uhuru kila mtu ndugu yake; nanyi mlikuwa mmefanya agano mbele zangu, katika nyumba ile iitwayo kwa jina langu;
16 lakini mlighairi, na kulitukana jina langu; kila mtu akamrudisha mtumwa wake na mjakazi wake, ambao mmewaweka huru kama walivyopenda wenyewe, mkawatia utumwani tena, wawe watumwa wenu na wajakazi wenu.
17 Basi BWANA asema hivi, Hamkunisikiliza kumtangazia uhuru kila mtu ndugu yake, na kila mtu jirani yake; tazama, mimi nawatangazieni uhuru, asema BWANA, yaani, wa upanga, na njaa, na tauni; nami nitawatoa ninyi mtupwe huko na huko katika falme zote za dunia.
18 Na watu hao waliolivunja agano langu, wasioyatimiza maneno ya agano lile, walilolifanya mbele zangu, wakati ule walipomkata ndama vipande viwili, wakapita katikati ya vipande vile;
19 wakuu wa Yuda, na wakuu wa Yerusalemu, matowashi, na makuhani, na watu wote wa nchi, waliopita katikati ya vipande vile vya huyo ndama;