2 Lakini yeye, wala watumishi wake, wala watu wa nchi, hawakuyasikiliza maneno ya BWANA aliyonena kwa kinywa cha nabii Yeremia.
3 Sedekia, mfalme, akamtuma Yehukali, mwana wa Shelemia, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, kwa Yeremia, nabii, kusema, Utuombee sasa kwa BWANA, Mungu wetu.
4 Basi Yeremia alikuwa akiingia na kutoka kati ya watu; kwa maana walikuwa hawakumfunga gerezani.
5 Na jeshi la Farao lilikuwa limetoka nchi ya Misri; na Wakaldayo waliohusuru Yerusalemu, waliposikia habari zao, wakavunja kambi yao mbele ya Yerusalemu.
6 Ndipo neno la BWANA likamjia nabii Yeremia, kusema,
7 BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mtamwambia hivi mfalme wa Yuda, aliyewatuma kwangu kuniuliza; Angalieni, jeshi la Farao, ambalo linakuja kuwasaidia, litarudi Misri, nchi yao wenyewe.
8 Na Wakaldayo watakuja tena, na kupigana na mji huu; nao watautwaa, na kuuteketeza.