2 nawe utaapa hivi, Kama BWANA aishivyo, katika kweli, na katika hukumu, na katika haki ndipo mataifa watajibariki katika yeye, nao watajitukuza katika yeye.
3 Maana BWANA awaambia hivi watu wa Yuda na Yerusalemu Ulimeni udongo katika konde zenu, wala msipande mbegu kati ya miiba.
4 Jitahirini kwa BWANA, mkaziondoe govi za mioyo yenu, enyi watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu; ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikawaka hata mtu asiweze kuizima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.
5 Tangazeni katika Yuda, hubirini katika Yerusalemu, na kusema, Pigeni baragumu katika nchi, pigeni kelele sana, na kusema, Jikusanyeni pamoja, tukaingie katika miji yenye boma.
6 Twekeni bendera kuelekea Sayuni; kimbieni mpate kuwa salama, msikawie; kwa maana nitaleta mabaya toka kaskazini, na maangamivu makuu.
7 Simba ametoka katika kichaka chake, ndiye aangamizaye mataifa; ameanza kushika njia, ametoka katika mahali pake; ili aifanye nchi yako kuwa ukiwa, miji yako ifanywe maganjo, asibaki mwenyeji ndani yake.
8 Kwa sababu hiyo jifungeni nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya BWANA haikugeuka na kutuacha.