Yer. 44:22-28 SUV

22 Hata BWANA asiweze kuvumilia tena, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu, na kwa sababu ya machukizo mliyoyafanya; kwa sababu hiyo nchi yenu imekuwa ukiwa, na ajabu, na laana, isikaliwe na mtu kama ilivyo leo.

23 Kwa sababu mmefukiza uvumba, na kwa sababu mmetenda dhambi juu ya BWANA, wala hamkuitii sauti ya BWANA, wala hamkwenda katika torati yake, wala katika amri zake, wala katika shuhuda yake; ndiyo maana mabaya haya yamewapata kama ilivyo leo.

24 Tena Yeremia akawaambia watu wote, na wanawake wote, Lisikieni neno hili la BWANA, ninyi nyote wa Yuda, mliopo hapa katika nchi ya Misri;

25 BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ninyi na wake zenu mmenena kwa vinywa vyenu, na kutimiza kwa mikono yenu, mkisema, Bila shaka tutazitimiza nadhiri zetu tulizoziweka, na kumfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kummiminia sadaka za kinywaji; basi, zithibitisheni nadhiri zenu, zitimizeni nadhiri zenu.

26 Basi, kwa sababu hiyo lisikieni neno la BWANA, ninyi nyote wa Yuda, mnaokaa katika nchi ya Misri, Tazama, nimeapa kwa jina langu kuu, asema BWANA, ya kwamba jina langu halitatajwa tena katika kinywa cha mtu awaye yote wa Yuda, katika nchi yote ya Misri, akisema, Kama Bwana MUNGU aishivyo!

27 Tazama, nawaangalia niwaletee mabaya, wala si mema; nao watu wote wa Yuda, waliopo hapa katika nchi ya Misri, wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa, hata wakomeshwe kabisa.

28 Nao watakaoukimbia upanga, watatoka katika nchi ya Misri, na kuiingia nchi ya Yuda, watu wachache sana; na wote wa Yuda waliosalia, waliokwenda nchi ya Misri ili kukaa huko, watajua ni neno la nani litakalosimama, neno langu, au neno lao.