1 Neno hili ndilo alilosema BWANA, katika habari za Babeli, na katika habari za Wakaldayo, kwa kinywa cha Yeremia, nabii.
2 Tangazeni katika mataifa,Mkahubiri na kutweka bendera;Hubirini, msifiche, semeni,Babeli umetwaliwa!Beli amefedheheka;Merodaki amefadhaika;Sanamu zake zimeaibishwa,Vinyago vyake vimefadhaika.
3 Maana toka kaskazini taifa linakuja juu yake, litakaloifanya nchi yake kuwa ukiwa; wala hapana mtu atakayekaa humo; wamekimbia, wamekwenda zao, mwanadamu na mnyama pia.
4 Katika siku hizo, na wakati huo, asema BWANA, wana wa Israeli watakuja, wao na wana wa Yuda pamoja; Wataendelea njiani mwao wakilia, nao watamtafuta BWANA, Mungu wao.
5 Watauliza habari za Sayuni, na nyuso zao zitaelekea huko, wakisema, Njoni ninyi, mjiunge na BWANA, kwa agano la milele ambalo halitasahauliwa.
6 Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea, wachungaji wao wamewapoteza; wamewapotosha milimani; wamekwenda toka mlima hata kilima, wamesahau mahali pao pa kupumzika.