38 Ukosefu wa mvua u juu ya maji yake, nayo yatakaushwa; maana ni nchi ya sanamu za kuchongwa, nao wameingiwa na wazimu kwa ajili ya sanamu.
39 Basi, wanyama wakali wa jangwani, pamoja na mbwa-mwitu, watakaa huko, na mbuni watakaa ndani yake; wala haitakaliwa na watu milele; wala hapana mtu atakayekaa huko tangu kizazi hata kizazi.
40 Kama vile vilivyotokea Mungu alipoangusha Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema BWANA; kadhalika hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama wageni wakaavyo.
41 Angalia, watu wanakuja watokao kaskazini; na taifa kubwa, na wafalme wengi wataamshwa toka pande za mwisho za dunia.
42 Wanashika upinde na mkuki;Ni wakatili, hawana huruma;Sauti yao inanguruma kama bahari,Nao wamepanda farasi;Kila mmoja amejipanga kama aendaye vitani,Juu yako, Ee binti Babeli.
43 Mfalme wa Babeli amesikia habari zao,Na mikono yake imekuwa dhaifu;Dhiki imemshika, na maumivu,Kama ya mwanamke katika utungu wake.
44 Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafula ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu?