4 Takaseni vita juu yake; inukeni, na tupande juu wakati wa adhuhuri. Ole wetu, kwa kuwa mchana umeanza kupungua, vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu.
5 Inukeni, na tupande juu wakati wa usiku, tukayaharibu majumba yake.
6 Maana BWANA wa majeshi asema hivi, Jikatieni miti, mfanyize boma juu ya Yerusalemu. Mji huu ni mji unaojiliwa; dhuluma tupu imo ndani yake.
7 Kama vile kisima kitoavyo maji yake, ndivyo utoavyo uovu wake; jeuri na kuharibu kwasikiwa ndani yake; ugonjwa na jeraha zi mbele zangu daima.
8 Uadhibishwe, Ee Yerusalemu, nafsi yangu, isije ikafarakana nawe; nisije nikakufanya ukiwa, nchi isiyokaliwa na watu.
9 BWANA wa majeshi asema hivi, Wataokota mabaki ya Israeli kama mzabibu; rudisha mkono wako ndani ya vikapu, kama mchuma zabibu.
10 Niseme na nani na kushuhudia, wapate kusikia? Tazama, sikio lao halikutahiriwa, wala hawawezi kusikiliza; tazama, neno la BWANA limekuwa matukano kwao; hawalifurahii.