9 Je! Nisiwapatilize kwa mambo hayo? Asema BWANA; na nafsi yangu je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?
10 Kwa milima nitalia na kulalama,Na kwa malisho ya nyikani nitafanya maombolezo;Kwa sababu yameteketea, hata hapana apitaye,Wala hapana awezaye kusikia sauti ya ng’ombe;Ndege wa angani, na wanyama wa mwituni,Wamekimbia, wamekwenda zao.
11 Nami nitafanya Yerusalemu kuwa magofu,Makao ya mbweha;Nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa,Isikaliwe na mtu awaye yote.
12 Ni nani aliye na hekima, apate kuelewa na haya? Tena ni nani ambaye kinywa cha BWANA kimesema naye, apate kuyatangaza? Nayo ni nini maana yake nchi hii kuharibika, na kuteketea kama nyika, asipite mtu?
13 Naye BWANA asema, Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu niliyoweka mbele yao, wala hawakuitii sauti yangu, wala kuenenda katika hiyo;
14 bali wameenenda katika ushupavu wa mioyo yao wenyewe, na kuandamana na Mabaali, kama walivyofundishwa na baba zao.
15 Basi, BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitawalisha pakanga, naam, watu hawa, nami nitawapa maji ya uchungu wayanywe.