12 Lakini mlipomwona mfalme Nahashi wa Waamoni amekuja kuwashambulia, mkamkataa Mwenyezi-Mungu ambaye ndiye Mfalme wenu, mkaniambia, ‘La! Mfalme ndiye atakayetutawala.’
13 Sasa, mfalme mliyejichagulia ndiye huyu hapa. Mlimwomba Mwenyezi-Mungu awape mfalme, naye amewapa.
14 Kama mkimcha Mwenyezi-Mungu, na kumtumikia, na kusikiliza sauti yake bila kuiasi amri yake, kama nyinyi wenyewe pamoja na mfalme anayewatawala mkimfuata Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, basi mtafanikiwa.
15 Lakini kama hamtasikiliza sauti ya Mwenyezi-Mungu, mkaasi amri yake, basi yeye atapambana nanyi pamoja na mfalme wenu.
16 Kwa hiyo basi, tulieni na kulitazama jambo hilo kubwa ambalo Mwenyezi-Mungu atatenda mbele yenu.
17 Je, sasa si wakati wa kuvuna ngano? Lakini mimi nitamwomba Mwenyezi-Mungu alete radi na mvua, nanyi mtatambua na kuona kuwa uovu wenu mliotenda mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa kujitakia mfalme, ni mkubwa.”
18 Basi, Samueli akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akatuma radi na mvua katika siku hiyo. Watu wote wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu na Samueli.