16 Kwa hiyo basi, tulieni na kulitazama jambo hilo kubwa ambalo Mwenyezi-Mungu atatenda mbele yenu.
17 Je, sasa si wakati wa kuvuna ngano? Lakini mimi nitamwomba Mwenyezi-Mungu alete radi na mvua, nanyi mtatambua na kuona kuwa uovu wenu mliotenda mbele ya Mwenyezi-Mungu kwa kujitakia mfalme, ni mkubwa.”
18 Basi, Samueli akamwomba Mwenyezi-Mungu, naye akatuma radi na mvua katika siku hiyo. Watu wote wakamwogopa sana Mwenyezi-Mungu na Samueli.
19 Hivyo wakamwambia Samueli, “Tafadhali utuombee sisi watumishi wako kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wako, ili tusife; kwa sababu tumezidisha dhambi zetu kwa uovu huo wa kujitakia mfalme.”
20 Samueli akawajibu, “Msiogope; ingawa mmefanya uovu huu, msiache kumfuata Mwenyezi-Mungu, ila mtumikieni kwa moyo wenu wote.
21 Msiifuate miungu ya uongo isiyo na faida wala haiwezi kuwaokoa, maana ni ya uongo.
22 Kwa heshima ya jina lake kuu, Mwenyezi-Mungu hatawatupa watu wake kwa sababu amependa kuwafanya nyinyi muwe watu wake.