9 Kisha, roho mbaya kutoka kwa Mwenyezi-Mungu alimjia Shauli alipokuwa amekaa nyumbani kwake akiwa ameshika mkuki mkononi, wakati ambapo Daudi alikuwa akipiga kinubi.
10 Shauli alijaribu kumchoma Daudi kwa mkuki huo, Lakini Daudi alikwepa mkuki wa Shauli na mkuki ukapiga ukuta. Daudi akakimbia na kutoroka.
11 Usiku huo, Shauli alituma watu nyumbani kwa Daudi wamwangalie kama yuko ili apate kumwua asubuhi. Lakini Mikali, mke wa Daudi akamwambia Daudi, “Kama huyasalimishi maisha yako usiku huu kesho utauawa.”
12 Hivyo Mikali akamteremsha Daudi kupitia dirishani, naye akatoka na kutoroka.
13 Mikali akachukua kinyago, akakilaza kitandani na kichwani pake akaweka mto wa manyoya ya mbuzi. Kisha akakifunika kwa nguo.
14 Shauli alipotuma watu kumshika Daudi, Mikali akawaambia kuwa Daudi ni mgonjwa.
15 Kisha Shauli aliwatuma warudi huko tena, akawaagiza akisema, “Mlete kwangu Daudi hata akiwa kitandani ili auawe.”