12 Watoto wa kiume wa Eli walikuwa walaghai sana. Hawakumjali Mwenyezi-Mungu
13 wala juu ya vitu ambavyo watu walipaswa kuwapa makuhani. Kila mara mtu alipokuwa anatolea tambiko yake, mtumishi wa kuhani alikuja na uma wenye meno matatu; na wakati nyama ikiwa bado inachemka,
14 huyo mtumishi aliuchomeka uma huo ndani ya chungu, nyama yoyote iliyotolewa humo na uma huo, ilikuwa mali ya kuhani. Waisraeli wote waliokwenda Shilo kutolea tambiko zao walitendewa hivyo.
15 Zaidi ya hayo, hata kabla mafuta hayajachomwa, mtumishi wa kuhani huja na kumwambia yule mtu anayetoa tambiko, “Mtolee kuhani nyama ya kubanika maana yeye hatapokea nyama yako iliyochemshwa, bali iliyo mbichi.”
16 Na kama mtu huyo akimjibu, “Ngojea kwanza nichome mafuta halafu utachukua kiasi chochote unachotaka,” hapo huyo mtumishi wa kuhani humjibu, “La, ni lazima unipe sasa hivi. La sivyo, nitaichukua kwa nguvu.”
17 Dhambi hii ya vijana hao wa Eli ilikuwa kubwa sana mbele ya Mwenyezi-Mungu. Maana, vijana hao walidharau matoleo ya Mwenyezi-Mungu.
18 Wakati huo, kijana Samueli aliendelea kumtumikia Mwenyezi-Mungu, akiwa amevaa kizibao cha kitani.