1 Siku ya tatu baadaye, Daudi na watu wake wakarudi Siklagi. Waamaleki walikuwa wamekwisha shambulia Negebu pamoja na mji wa Siklagi na kuuteketeza kwa moto.
2 Walikuwa wameteka wanawake na watu wote waliokuwa mjini humo, wakubwa kwa wadogo. Hao waliowateka, waliondoka nao wakiwa hai, bila ya kumwua mtu yeyote.
3 Daudi na watu wake walipofika mjini waliukuta mji umeteketezwa, na wanawake, watoto wao wa kiume na wa kike, wamechukuliwa mateka.
4 Ndipo Daudi na watu wake walipoangua kilio, wakalia hadi walipoishiwa nguvu.
5 Wake wawili wa Daudi, Ahinoamu kutoka Yezreeli na Abigaili mjane wa Nabali, nao pia walikuwa wamechukuliwa mateka.
6 Sasa, Daudi alikuwa katika matatizo makubwa kwa kuwa watu wake walikuwa na uchungu rohoni mwao kwa kupoteza watoto wao; hivyo wakawa wanamtishia kumpiga mawe. Lakini Daudi alijipa moyo kwa kumtegemea Mwenyezi-Mungu, Mungu wake.
7 Daudi akamwambia kuhani Abiathari mwana wa Ahimeleki, “Niletee kizibao cha kuhani.” Abiathari akampelekea.