1 Katika mwaka wa ishirini na tatu wa enzi ya mfalme Yoashi wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala Israeli, akaendelea kutawala huko Samaria muda wa miaka kumi na saba.
2 Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu kama vile mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati aliyewakosesha watu wa Israeli wakatenda dhambi. Yehoahazi hakuacha matendo hayo mabaya.
3 Mwenyezi-Mungu alikasirika, akawafanya watu wa Israeli washindwe vitani mara kwa mara na mfalme Hazaeli wa Aramu na mwanawe Ben-hadadi.
4 Yehoahazi akamsihi Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu alipoona jinsi mfalme wa Aramu alivyowadhulumu watu wa Israeli alisikia maombi yake.