14 Kwa hiyo kuhani Hilkia, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya, wote walikwenda kwa mama mmoja nabii jina lake Hulda aliyekuwa mke wa Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya hekalu. Wakati huo Hulda alikuwa anaishi katika mtaa wa pili wa Yerusalemu, nao wakazungumza naye.
15 Basi akawaambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Mwambie huyo aliyewatuma kwangu,
16 Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Nitaleta uovu juu ya mahali hapa na juu ya wakazi wake kama ilivyo katika kitabu kilichosomwa na mfalme wa Yuda.
17 Kwa sababu wameniacha na kufukizia ubani miungu mingine na hivyo kunikasirisha kwa kazi zote za mikono yao, ghadhabu yangu dhidi ya Yerusalemu itawaka na haitaweza kutulizwa.
18 Lakini kuhusu mfalme wa Yuda aliyewatuma kutafuta shauri la Mwenyezi-Mungu, mwambie kwamba, hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, juu ya maneno uliyoyasikia,
19 Kwa kuwa umetubu na kunyenyekea mbele yangu, hata umerarua mavazi yako na kulia mbele yangu, hapo uliposikia niliyosema dhidi ya mahali hapa na dhidi ya wakazi wake, ya kwamba watakuwa ukiwa na laana, nami pia nimekusikia.
20 Kwa hiyo tazama, nitakukusanya pamoja na babu zako nawe utawekwa kaburini kwa amani, macho yako hayataona uovu nitakaouleta juu ya mahali hapa.’” Basi wajumbe wakamletea mfalme Yosia habari hizi.