5 Kiasi cha fedha hizo zipewe wasimamizi wa marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kulipa mishahara ya mafundi wanaofanya marekebisho,
6 yaani maseremala, wajenzi na waashi. Kiasi kingine kitumike kununua mbao na mawe yaliyochongwa kwa ajili ya kurekebisha nyumba.
7 Watu wanaosimamia ujenzi wasidaiwe kutoa hesabu ya matumizi ya fedha watakazokabidhiwa, kwa sababu wanazitumia kwa uaminifu.”
8 Kisha kuhani mkuu Hilkia alimwambia katibu Shafani, “Nimekipata Kitabu cha Sheria katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Halafu Hilkia akampatia Shafani kitabu, naye akakisoma.
9 Katibu Shafani, alimwendea mfalme na kutoa habari, akisema, “Watumishi wako wametoa fedha zilizopatikana katika nyumba halafu wamezikabidhi kwa mafundi wanaosimamia marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.”
10 Kisha katibu Shafani, akamwambia mfalme, “Kuhani Hilkia amenipa kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme.
11 Mfalme aliposikia maneno ya Kitabu cha Sheria, alirarua mavazi yake.