2 Basi, Mwenyezi-Mungu akampelekea makundi ya Wababuloni, Waaramu, Wamoabu na Waamoni washambulie nchi ya Yuda na kuiharibu, kulingana na neno la Mwenyezi-Mungu alilolisema kwa watumishi wake manabii.
3 Hakika mambo haya yaliikumba nchi ya Yuda kwa amri ya Mwenyezi-Mungu, ili kuwahamisha kutoka mbele yake, kwa sababu ya dhambi za mfalme Manase na yote aliyoyatenda,
4 na kwa sababu ya damu isiyo na hatia aliyoimwaga. Mwenyezi-Mungu hakumsamehe makosa hayo.
5 Basi matendo mengine ya Yehoyakimu na yote aliyoyafanya yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda.
6 Yehoyakimu akafariki, na mwanawe Yehoyakini akatawala mahali pake.
7 Mfalme wa Misri hakutoka tena nchini kwake, kwa sababu mfalme wa Babuloni aliitwaa na kuimiliki nchi yote iliyokuwa chini ya mfalme wa Misri hapo awali tangu kijito cha Misri mpaka mto Eufrate.
8 Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; alitawala huko Yerusalemu kwa muda wa miezi mitatu. Mama yake alikuwa Nehushta binti Elnathani, mkazi wa Yerusalemu.