22 Walipoamka asubuhi iliyofuata, jua lilikuwa linametameta juu ya maji hayo; walipoyatazama yakaonekana kuwa mekundu kama damu.
23 Wakasema, “Hii ni damu! Bila shaka hawa wafalme watatu wamepigana wao kwa wao na kuuana! Twendeni tukachukue nyara!”
24 Lakini walipofika katika kambi ya Israeli, watu wa Israeli waliwashambulia, nao wakakimbia mbele yao. Watu wa Israeli wakawafuatia mpaka Moabu huku wakiwaua
25 na kuibomoa miji yao. Kila walipopita penye shamba zuri, kila mtu alilirushia jiwe mpaka kila shamba likajaa mawe; kadhalika wakaziziba chemchemi zote za maji na kukata miti yote mizuri. Hatimaye, ukabaki mji mkuu wa Kir-haresethi peke yake, ambao pia wapiga kombeo waliuzingira na kuuteka.
26 Mfalme wa Moabu alipoona kwamba vita vinamwendea vibaya, alichukua watu wake 700 wenye kupigana kwa mapanga, akikusudia kupenya majeshi ya adui zake mkabala na mfalme wa Edomu, lakini hakufaulu.
27 Hapo akamchukua mwanawe wa kwanza ambaye angekuwa mfalme mahali pake, akamtoa kuwa sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta wa mji. Watu wa Israeli walipoona hayo, wakachukizwa mno. Wakauacha mji huo na kurudi nchini kwao.