10 Mtauawa kwa upanga, nami nitawahukumu mpakani mwa Israeli. Hapo ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
11 Mji wa Yerusalemu hautakuwa tena chungu chenu wala nyinyi hamtakuwa nyama ndani yake. Mimi nitawahukumu mpakani mwa Israeli.
12 Nanyi mtatambua kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu ambaye sheria zake hamkuzifuata na maagizo yake hamkutekeleza, bali mmetenda kulingana na maagizo ya mataifa yanayowazunguka.”
13 Nilipokuwa natabiri, Pelatia mwana wa Benaya akafariki. Nami nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kubwa, nikisema, “Ee Bwana Mwenyezi-Mungu, je, utawamaliza kabisa Waisraeli waliobaki?”
14 Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
15 “Wewe mtu, ndugu zako na wakazi wa Yerusalemu ambao pia ni ndugu zako wanasema juu yako na juu ya watu wote wa Israeli walioko uhamishoni, ‘Nyinyi mlio uhamishoni mko mbali sana na Mwenyezi-Mungu; maana Mwenyezi-Mungu ametupa sisi nchi hii iwe mali yetu.’
16 “Lakini, waambie hao walio uhamishoni kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ingawa nimewapeleka mbali miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi nyingine, hata hivyo, kwa wakati uliopo mimi nipo pamoja nao huko waliko.