1 Mwenyezi-Mungu aliniambia: “Wewe mtu! Toa unabii kuhusu milima ya Israeli. Iambie isikilize maneno yangu
2 mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Maadui zenu wamewazomea na kusema kuwa nyinyi mmekuwa mali yao!
3 “Kwa hiyo, wewe Ezekieli, toa unabii useme kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Watu wamewafanya nyinyi milima ya Israeli kuwa tupu na kuwavamia kutoka kila upande hata mmekuwa mali ya mataifa mengine, mkawa kitu cha kusimangwa na kudhihakiwa miongoni mwa watu!
4 Kwa hiyo, enyi milima ya Israeli, sikieni neno langu mimi Bwana Mwenyezi-Mungu: Nyinyi milima na vilima, mifereji na mabonde, nyika tupu na miji mmehamwa, mkatekwa nyara na kudharauliwa na mataifa yote yanayowazungukeni.
5 Sasa kwa kuwa mimi nimechukizwa mno, nitayaadhibu mataifa mengine na hasa watu wa Edomu. Wao kwa furaha moyoni na madharau waliichukua hiyo nchi iliyo yangu iwe yao.
6 Kwa hiyo, ewe mtu, toa unabii kuhusu nchi ya Israeli, uiambie milima na vilima, vijito na mabonde kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema mambo haya kutokana na ghadhabu yangu yenye wivu juu ya nchi yangu, kwa sababu imetukanwa na watu wa mataifa.
7 Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ninaapa kwamba watu wa mataifa yaliyo jirani nanyi watatukanwa wao wenyewe.
8 “Lakini kuhusu milima ya Israeli, miti itatoa matawi na kuzaa matunda kwa ajili ya watu wangu wa Israeli, maana wao watarudi makwao karibuni.
9 Mimi niko upande wenu, nitahakikisha kuwa mnalimwa na kupandwa mbegu.
10 Waisraeli nitawazidisha sana. Miji itakaliwa, na magofu yatajengwa upya.
11 Nitawafanya watu na wanyama waongezeke na kuwa wengi. Nitawafanya nyinyi milima mkaliwe tena kama zamani. Nitawatendea mema mengi kuliko zamani. Nanyi mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
12 Nitawafanya watu wangu Israeli watembee juu yenu. Nanyi mtakuwa milki yao, wala hamtawafanya tena wafiwe na watoto wao.
13 “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Kwa vile watu wamesema juu yenu kwamba mnakula watu, na mmelipokonya taifa lenu watoto wake,
14 basi, sasa hamtakula tena watu wala kupokonya taifa lenu watoto wake. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.
15 Sitaruhusu tena mataifa yawatukane, wala kuwadharau tena. Hamtasababisha taifa lenu likose. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”
16 Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
17 “Wewe mtu! Waisraeli walipoishi katika nchi yao waliitia unajisi kwa mienendo na matendo yao. Niliyaona matendo yao kuwa sawa na mwanamke aliye najisi wakati wa siku zake.
18 Niliwamwagia ghadhabu yangu kwa sababu ya damu waliyomwaga katika nchi na kwa sababu ya miungu ambayo kwayo nchi ilitiwa unajisi.
19 Niliwatawanya kati ya mataifa, wakasambazwa katika nchi nyingine. Niliwaadhibu kadiri ya tabia yao na matendo yao.
20 Hata walipokuwa miongoni mwa mataifa walilikufuru jina langu takatifu, hata watu wakasema hivi juu yao: ‘Tazama! Hawa ndio wale watu wa Mwenyezi-Mungu, lakini wamelazimika kuondoka katika nchi yake!’
21 Hiyo ilinifanya kuhangaika juu ya jina langu takatifu ambalo watu wa Israeli walilikufuru miongoni mwa mataifa walikokwenda.
22 Basi, waambie Waisraeli kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ninachotaka kufanya si kwa faida yenu nyinyi watu wa Israeli, bali ni kwa heshima ya jina langu takatifu mlilolikufuru miongoni mwa mataifa mlikokwenda.
23 Nitalirudishia hadhi yake takatifu jina langu kuu mlilokufuru miongoni mwa mataifa. Hapo ndipo mataifa yatakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Nitawatumia nyinyi kuonesha utakatifu wangu mbele yao.
24 Nitawaondoa nyinyi katika kila taifa na kuwakusanya kutoka nchi zote za kigeni; nitawarudisha katika nchi yenu wenyewe.
25 Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtatakata uchafu wenu wote na sanamu za miungu yenu yote.
26 Nitawapeni moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu. Nitauondoa kwenu moyo mgumu kama jiwe na kuwapa moyo wa utii.
27 Nitatia roho yangu ndani yenu; nitawafanya mfuate kanuni zangu na kuzingatia maazimio yangu.
28 Mtakaa katika nchi niliyowapa wazee wenu. Mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.
29 Nitawaokoa kutoka uchafu wenu wote. Nitaiamuru ngano iongezeke, wala sitawaletea njaa tena.
30 Nitayazidisha matunda ya miti na mazao ya mashamba ili msiaibike tena kwa njaa kati ya mataifa.
31 Kisha mtakapokumbuka mienendo yenu miovu na matendo yenu mabaya, mtajichukia wenyewe kwa sababu ya maovu yenu na machukizo mliyofanya.
32 Lakini jueni kwamba sitafanya hivyo kwa ajili yenu. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema. Oneni aibu na kufadhaika kwa sababu ya matendo yenu, enyi Waisraeli!
33 “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile nitakapowasafisheni maovu yenu yote, nitaifanya miji yenu ikaliwe, nayo magofu yajengwe upya.
34 Nchi iliyokuwa jangwa italimwa tena, hata atakayepita huko hataiona kuwa jangwa.
35 Nao watu watasema: ‘Nchi hii iliyokuwa jangwa, sasa imekuwa kama bustani ya Edeni, nayo miji iliyokuwa ukiwa, mahame na magofu, sasa inakaliwa na watu, tena ina ngome!’
36 Hapo mataifa yaliyobaki kandokando yenu, yatatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu niliyejenga upya yaliyoharibiwa na kupanda mbegu katika nchi iliyokuwa jangwa. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema, na nitafanya hayo.
37 “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Waisraeli wataniomba niwafanye kuwa wengi kama kundi la kondoo, nami nitawafanya hivyo.
38 Wataniomba wawe wengi kama kundi la kondoo wa tambiko, naam, kama kundi la kondoo mjini Yerusalemu wakati wa sikukuu zake. Hivyo ndivyo miji yenu iliyokuwa ukiwa itakavyojaa makundi ya watu. Hapo ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”