1 Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
2 “Wewe mtu, igeukie milima ya Israeli, utangaze ujumbe huu wangu dhidi ya wakazi wake
3 na kusema: Sikilizeni neno la Bwana Mwenyezi-Mungu enyi wakazi wa milima ya Israeli: Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nawaambieni nyinyi wakazi wa milimani na vilimani, wa magengeni na mabondeni kwamba mimi mwenyewe nitaleta upanga na kuharibu sehemu zenu zote zilizoinuka za ibada.
4 Madhabahu zenu zitaharibiwa na mahali penu pa kufukizia ubani patavunjwavunjwa. Wale watakaouawa nitawatupa mbele ya sanamu zenu za miungu.
5 Maiti za Waisraeli nitazilaza mbele ya sanamu zao za miungu, na mifupa yenu nitaitawanya kandokando ya madhabahu zenu.
6 Kokote mnakoishi, miji yenu itakuwa ukiwa na sehemu za mwinuko za ibada zenu zitabomolewa, madhabahu zenu ziwe uharibifu na maangamizi, sanamu zenu za miungu zivunjwe na kuharibiwa. Mahali penu pa kufukizia ubani patabomolewa na chochote mlichofanya kitatokomezwa.
7 Wale watakaouawa wataanguka kati yenu, nanyi mtatambua kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu.
8 “Hata hivyo, nitawaacha wengine wabaki hai; baadhi yenu watanusurika kuuawa nao watatawanyika katika nchi mbalimbali.
9 Ndipo watakaponikumbuka mimi miongoni mwa hao watu wa mataifa ambamo watatawanyika. Watakumbuka jinsi nilivyowapiga kwa sababu mioyo yao isiyo na uaminifu ilinigeuka na kwa vile waliacha kunitazamia mimi wakazitazamia sanamu za miungu. Kwa hiyo watajichukia wao wenyewe kwa sababu ya maovu na machukizo yao yote waliyoyatenda.
10 Hapo ndipo watakapojifunza kwamba mimi ni Mwenyezi-Mungu; sikuwatisha bure ya kwamba nitawaletea maovu hayo yote.”
11 Bwana Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Piga makofi, piga kishindo kwa mguu na kusema: Ole wenu Waisraeli kwa sababu ya machukizo yenu yote, kwani mtakufa kwa upanga, njaa na kwa maradhi mabaya.
12 Aliye mbali sana atakufa kwa maradhi mabaya. Aliye karibu atauawa kwa upanga. Atakayekuwa amebaki na kunusurika hayo mawili atakufa kwa njaa. Ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu dhidi yao.
13 Maiti zao zitatapakaa kati ya sanamu zao za miungu na madhabahu zao, juu ya kila mlima, chini ya kila mti mbichi, chini ya kila mwaloni wenye majani na kila mahali walipotolea tambiko zao za harufu nzuri ya kuzipendeza sanamu zao za miungu. Hapo ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.
14 Nitaunyosha mkono wangu dhidi yao, na kuiharibu nchi yao. Tangu huko jangwani kusini mpaka mjini Ribla kaskazini, nitaifanya nchi yao kuwa mahame kabisa wasipate mahali pa kuishi. Hapo ndipo wote watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”