Ezekieli 32 BHN

Farao analinganishwa na mamba

1 Siku ya kwanza ya mwezi wa kumi na mbili, mwaka wa kumi na mbili tangu uhamisho wetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

2 “Wewe mtu! Imba utenzi wa kuomboleza juu ya Farao, mfalme wa Misri.Wewe Farao unajiona kuwa simba kati ya mataifa,lakini wewe ni kama mamba tu majini:Unachomoka kwa nguvu kwenye mito yako,wayavuruga maji kwa miguu yako,na kuichafua mito.

3 Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema:Nitautupa wavu wangu juu yako,nao watu watakuvua humo kwa wavu wangu.

4 Nitakutupa juu ya nchi kavu,nitakubwaga uwanjani,nitawafanya ndege wote watue juu yako,na kuwashibisha wanyama wote wa porini kwa mwili wako.

5 Nitatawanya nyama yako milimani,na kujaza mabonde yote mzoga wako.

6 Nchi nitainywesha damu yako mpaka milimani,mashimo yatajaa damu yako.

7 Nitakapokuangamiza, nitazifunika mbingu,nitazifanya nyota kuwa nyeusi,jua nitalifunika kwa mawingu,na mwezi hautatoa mwangaza wake.

8 Nitaifanya mianga yote mbinguni kuwa giza,nitatandaza giza juu ya nchi.Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.

9 “Nitaihuzunisha mioyo ya watu wengi, nitakapokupeleka utumwani kati ya mataifa, katika nchi ambazo huzijua.

10 Nitayashtusha mataifa mengi kwa habari zako,wafalme wao watatetemeka kwa sababu yako,nitakaponyosha upanga wangu mbele yao.Watatetemeka kila wakati,kila mtu akihofia uhai wake,siku ile ya kuangamia kwako.

11 Kwa maana, mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:Upanga wa mfalme wa Babuloni utakufuatia.

12 Watu wako wengi watauawa kwa mapanga ya mashujaa,watu katili kuliko mataifa yote.Watakomesha kiburi cha Misri na kuwaua watu wako wote.

13 Nitaiangamiza mifugo yako yote kando ya mto Nili.Maji yake hayatavurugwa tena na mtuwala kwato za mnyama kuyachafua tena.

14 Hapo nitayafanya maji yake yatuliena kuitiririsha mito yake kama mafuta.Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.

15 “Nitakapoifanya nchi ya Misri kuwa jangwa na mali yake yote kuchukuliwa, nitakapowaua wakazi wake wote, ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.

16 “Huo ndio utenzi wa maombolezo,wanawake wa mataifa watauimba,wataimba juu ya Misri na watu wake wote.Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nimesema.”

Nchi ya wafu

17 Siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza, mwaka wa kumi na mbili tangu kuhamishwa kwetu, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

18 “Wewe mtu! Waombolezee watu wengi wa Misri. Wapeleke chini kwenye nchi ya wafu pamoja na mataifa mengine yenye nguvu, waende huko pamoja nao washukao chini kwa wafu.

19 Waambie:Nyinyi ni wazuri kuliko nani?Nendeni kuzimu mlazwe pamoja na wasiomjua Mungu!

20 Watu wa Misri wataangamia pamoja na watu waliouawa vitani. Upanga uko tayari kuangamiza Misri pamoja na watu wake wengi.

21 Wakuu wenye nguvu pamoja na wasaidizi wao wakiwa huko shimoni kwa wafu watasema hivi: ‘Wamisri wameshuka chini kwa wafu, wanalala pamoja na watu wasiomjua Mungu, waliouawa vitani.’

22 “Waashuru wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao. Wote waliuawa vitani,

23 na makaburi yao yako sehemu za chini kabisa shimoni kwa wafu. Wanajeshi wao wote waliuawa vitani na makaburi yao yamewazunguka. Hapo awali, walipokuwa wanaishi bado, walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai.

24 “Waelamu pia wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao waliouawa vitani. Wote hao wasiomjua Mungu walishuka kwenye nchi ya wafu. Walipokuwa wanaishi bado walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai. Lakini sasa wanabeba aibu yao pamoja na wanaoshuka shimoni kwa wafu.

25 Wamelazwa na jeshi lao miongoni mwa wale waliouawa vitani. Wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wake wote waliouawa vitani na ambao wote hawamjui Mungu. Walipokuwa bado wanaishi walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai, na sasa wako hapo wamejaa aibu pamoja na wale waliouawa vitani.

26 “Watu wa Mesheki na wa Tabali wote wako huko, wamezungukwa na makaburi ya wanajeshi wao. Watu hao wote wasiomjua Mungu walikufa vitani, watu ambao walipokuwa hai walieneza vitisho vyao katika nchi ya walio hai.

27 Hao wasiomjua Mungu hawakuzikwa pamoja na mashujaa wa kale, ambao walikwenda kuzimu kwa wafu wakiwa na silaha zao, mapanga yao chini ya vichwa vyao na ngao zao juu ya miili yao. Mashujaa hao walipokuwa wanaishi bado walijaza vitisho vyao katika nchi ya walio hai.

28 Basi, nyinyi Wamisri mtaangamizwa na kulazwa miongoni mwa wasiomjua Mungu waliouawa vitani.

29 “Waedomu wako huko pamoja na wafalme wao na wakuu wao wote. Walipokuwa bado hai walikuwa na nguvu sana, lakini sasa wamelazwa kwa wafu pamoja na wasiomjua Mungu waliouawa vitani.

30 “Viongozi wote wa watu wa kaskazini wako huko pia; hata Wasidoni wote walikwenda kujiunga na wafu. Walipokuwa bado wanaishi, walisababisha vitisho kwa nguvu zao, lakini sasa hao wasiomjua Mungu wamelazwa chini kwa aibu pamoja na wale waliouawa vitani. Wanashiriki aibu ya wale walioshuka shimoni kwa wafu.

31 “Farao, atakapowaona hao wote atafarijika kwa ajili ya wingi wa majeshi yake yote; mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.

32 Nilimfanya Farao aeneze vitisho katika nchi ya walio hai, lakini sasa yeye mwenyewe pamoja na jeshi lake lote watauawa vitani na kulazwa pamoja na wasiomjua Mungu, waliokufa vitani. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”