1 Naye akaniambia, “Wewe mtu! Simama wima. Nataka kuongea nawe.”
2 Alipokuwa akiongea nami, roho ya Mungu ikaniingia na kunisimamisha wima. Ndipo nikamsikia
3 akiniambia, “Wewe mtu nakutuma kwa Waisraeli, taifa la waasi ambao wameniasi. Wameendelea kunikosea mimi hadi leo kama walivyokuwa wazee wao.
4 Watu hao ni wafidhuli na wajeuri. Nakutuma kwao, nawe utawaambia kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi na hivi.
5 Wakisikia au wasiposikia, maana wao ni watu waasi, walau watatambua kwamba nabii amekuwapo miongoni mwao.
6 Lakini, ewe mtu usiwaogope hao wala maneno yao. Hata kama mbigili na miiba vinakuzunguka, au unaketi juu ya nge, usiogope maneno yao wala usitishwe na nyuso zao, kwani hao ni watu waasi.
7 Wewe utawaambia maneno yangu, hata kama watasikia au hawatasikia, maana wao ni watu waasi.
8 “Lakini ewe mtu, sikiliza ninayokuambia, wala usiwe mwasi kama watu hao. Fumbua kinywa chako, ule ninachokupa.”
9 Nilipotazama, niliona nimenyoshewa mkono, na kumbe ulikuwa na kitabu kilichoandikwa.
10 Basi akakifungua mbele yangu, nacho kilikuwa kimeandikwa mbele na nyuma maneno ya maombolezo, vilio na laana.