Ezekieli 48 BHN

Eneo la makabila huko Kaskazini

1 Haya ndiyo majina ya makabila na sehemu zao: Kuanzia mpaka wa kaskazini kwenye barabara ya Hethloni hadi kuingia Hamathi hadi mji wa Hazar-enoni (ulioko mpakani mwa Damasko na Hamathi upande wa kaskazini na kuendelea kutoka mashariki hadi magharibi), eneo hilo litakuwa la kabila la Dani.

2 Eneo linalopakana na la Dani, kutoka mashariki hadi magharibi litakuwa la Asheri.

3 Kabila la Naftali, litapata eneo linalopakana na lile la Asheri, kutoka mashariki hadi magharibi.

4 Baada ya eneo la kabila la Naftali, litafuata eneo la kabila la Manase, kutoka mashariki hadi magharibi.

5 Eneo linalopakana na eneo la Manase, kutoka upande wa mashariki hadi magharibi, litakuwa la kabila la Efraimu.

6 Eneo linalopakana na eneo la Efraimu, kutoka mashariki hadi magharibi, litakuwa la kabila la Reubeni.

7 Eneo linalopakana na eneo la Reubeni, kutoka mashariki hadi magharibi litakuwa la kabila la Yuda.

Eneo maalumu katikati ya nchi

8 Baada ya eneo la kabila la Yuda, utatenga eneo lenye urefu wa kilomita 12 na upana kama huohuo, kutoka kaskazini hadi kusini, na urefu huohuo kutoka mashariki hadi magharibi, sawasawa na eneo la kabila lolote. Hapo katikati ya eneo hilo patakuwa na maskani ya Mungu.

9 Eneo utakalotenga kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu litakuwa lenye urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kwa kilomita 10.

10 Makuhani watakuwa na eneo lao katika eneo hilo. Eneo hilo litakuwa na urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kutoka mashariki hadi magharibi, na kilomita 5 kutoka kaskazini hadi kusini. Maskani ya Mungu itakuwa katikati ya eneo hilo.

11 Eneo hilo litakuwa kwa ajili ya makuhani wa wazawa wa Sadoki, ambao walinitumikia kwa uaminifu na hawakuasi wakati Waisraeli walipoasi kama Walawi walivyofanya.

12 Hilo litakuwa eneo lao maalumu kutoka katika eneo takatifu la nchi, eneo takatifu kabisa, litakalopakana na eneo la Walawi.

13 Nao Walawi, eneo lao litakuwa kusini mwa eneo la makuhani. Eneo hilo litakuwa na urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu kutoka mashariki hadi magharibi, na upana kilomita 5 kutokea kaskazini hadi kusini.

14 Hakuna sehemu yoyote ya eneo hilo itakayouzwa au kutolewa kwa mtu yeyote, kwa sababu eneo hilo ni takatifu kwa Mwenyezi-Mungu; nalo ni bora kuliko yote nchini.

15 Ile sehemu ya eneo maalumu iliyobaki, yenye urefu wa kilomita kumi na mbili u nusu na upana kilomita 2.5, hilo ni kwa matumizi ya kawaida ya mji: Mahali pa kuishi na eneo la mashamba. Katikati yake kutakuwa na mji,

16 nao utakuwa wa mraba, kila upande mita 2,250.

17 Kuuzunguka mji, kutakuwa na eneo wazi lenye upana wa mita 125.

18 Eneo ambalo litabaki baada ya kujengwa hekalu, kusini mwa mji, kilomita 5 kwa kilomita 2.5, upande wa mashariki, na kilomita 5 kwa kilomita 2.5 upande wa magharibi, litakuwa eneo la wakulima kwa wakazi wa mji.

19 Wafanyakazi wa mjini wa kabila lolote la Israeli wanaweza kulima katika eneo hilo.

20 Hivyo, eneo lote utakalotenga, yaani eneo takatifu pamoja na eneo la mji, litakuwa la mraba, kilomita kumi na mbili u nusu kila upande.

21 Eneo linalosalia katika pande zote za eneo takatifu na eneo la mji, yaani lile eneo lenye eneo mraba likiwa na kilomita kumi na mbili u nusus kwa kila upande tokea mashariki hadi magharibi, mkabala na maeneo ya makabila, litakuwa la mtawala. Lile eneo takatifu ambamo maskani ya Mungu itakuwa katikati yake,

22 na eneo la Walawi pamoja na lile eneo la mji, yatakuwa katikati ya eneo la mtawala. Eneo la mtawala litakuwa katika mpaka wa eneo la kabila la Yuda na eneo la kabila la Benyamini.

Ardhi ya makabila mengine

23 Makabila yaliyobaki yatagawiwa maeneo yao hivi: Kabila la Benyamini litapewa eneo kutoka mashariki hadi magharibi.

24 Eneo linalopakana na eneo la Benyamini kutoka upande wa mashariki kuelekea upande wa magharibi litakuwa la kabila la Simeoni.

25 Eneo linalopakana na kabila la Simeoni kutoka upande wa mashariki kuelekea upande wa magharibi litakuwa eneo la kabila la Isakari.

26 Eneo linalopakana na kabila la Isakari kutoka upande wa mashariki kuelekea upande wa magharibi, litakuwa eneo la kabila la Zebuluni.

27 Eneo linalopakana na kabila la Zebuluni, kutoka mashariki kuelekea magharibi, litakuwa eneo la kabila la Gadi.

28 Eneo linalopakana na kabila la Gadi kuelekea kusini, mpaka utatoka mji wa Tamari hadi kwenye chemchemi za Meriba-kadeshi na kupitia upande wa mashariki ya Misri hadi Bahari ya Mediteranea.

29 Hilo ndilo eneo la makabila ya Israeli. Humo ndimo watapewa maeneo yao, kila kabila eneo lake. Bwana Mwenyezi-Mungu amesema.

Malango ya Yerusalemu

30 Mji wa Yerusalemu utakuwa na ukuta ambao utakuwa na malango haya ya kutokea na kuingia: Upande wa kaskazini urefu wa ukuta utakuwa mita 2,250. Upande huo wa kaskazini

31 utakuwa na malango matatu: Lango la Reubeni, lango la Yuda na lango la Lawi.

32 Ukuta wa Mashariki utakuwa na urefu wa mita 2,250. Upande huo utakuwa na malango matatu: Lango la Yosefu, lango la Benyamini na lango la Dani.

33 Ukuta wa upande wa kusini utakuwa na urefu wa mita 2,250. Upande huo utakuwa na malango matatu: Lango la Simeoni, lango la Isakari na lango la Zebuluni.

34 Ukuta wa upande wa magharibi utakuwa na urefu wa mita 2,250. Upande huo nao utakuwa na malango matatu: Lango la Gadi, lango la Asheri na lango la Naftali.

35 Jumla ya urefu wa kuta zote nne utakuwa ni mita 9,000. Jina la mji kutokea sasa na kuendelea litakuwa: “Mwenyezi-Mungu Yupo Hapa.”