Ezekieli 7 BHN

Mwisho wa Israeli ni karibu

1 Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

2 “Wewe mtu, waambie wakazi wa nchi ya Israeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi:Sasa ni mwisho!Mwisho umeifikia nchi yote kutoka pande zote nne!

3 Sasa mwisho umewafikia;sasa mtausikia ukali wa hasira yangu juu yenu.Nitawahukumu kadiri ya mwenendo wenu.Nitawaadhibu kwa machukizo yenu yote.

4 Sitawaachia wala sitawahurumia;nitawaadhibu kulingana na mienendo yenu,maadamu machukizo bado yapo kati yenu.Ndipo mtakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.

5 Ninachosema mimi Bwana Mwenyezi-Mungu ni hiki:Mtapatwa na maafa mfululizo!

6 Mwisho umekuja!Naam, mwisho umefika!Umewafikia nyinyi!

7 Enyi wakazi wa nchi hii, maangamizi yenu yamewajia!Wakati umekuja;naam, siku imekaribia.Hiyo ni siku ya msukosukona siyo ya sauti za shangwe mlimani.

8 Sasa mtausikia uzito wa hasira yangu juu yenu.Nitawahukumu kulingana na mwenendo wenu;nitawaadhibu kadiri ya machukizo yenu.

9 Sitawaachilia wala sitawaonea huruma.Nitawaadhibu kulingana na mienendo yenumaadamu machukizo yapo bado miongoni mwenu.Ndipo mtakapotambua kuwa ni mimi Mwenyezi-Mungu ninayewaangamiza.

10 “Tazameni, siku ile inakuja!Maangamizi yenu yamekuja.Ukatili uko kila mahali na kiburi kimechanua.

11 Ukatili unaendelea kuwa mbaya zaidi.Hakuna hata mmoja wenu atakayebaki,wala vitu mlivyojirundikia kwa wingi au utajiri wenu;hatakuwako mtu mwenye heshima miongoni mwenu.

12 Wakati umewadia,naam, ile siku imekaribia.Mnunuzi asifurahi wala mwuzaji asiomboleze;kwa sababu ghadhabu yangu itaukumba umati wote.

13 Wauzaji hawataweza kurudia mali yao waliyouzahata kama wakibaki hai.Kwani maono haya yahusu umati wote na hayatabatilishwa.Kutokana na uovu huo, hakuna mtu atakayesalimisha maisha yake.

14 Tarumbeta imepigwa na kuwafanya wote wawe tayari.Lakini hakuna anayekwenda vitani,kwani ghadhabu yangu iko juu ya umati wote.

15 Nje kuna kifo kwa upangana ndani ya mji kuna maradhi mabaya na njaa.Walioko shambani watakufa kwa upanga;walio mjini njaa na maradhi mabaya yatawaangamiza.

16 Wakiwapo watu watakaosalimikawatakimbilia milimani kama hua waliotishwa bondeni.Kila mmoja wao ataomboleza kwa dhambi zake.

17 Kila mtu, mikono yake itakuwa dhaifuna magoti yake yatakuwa maji.

18 Watavaa mavazi ya gunia,hofu itawashika,nao watakuwa na aibu,vichwa vyao vyote vitanyolewa.

19 Watatupa fedha yao barabaranina dhahabu yao itakuwa kama kitu najisi.Fedha na dhahabu zao hazitaweza kuwaokoakatika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu;wala hawataweza kushibaau kuyajaza matumbo yao fedha na dhahabu waliyojirundikia;kwani mali hiyo ndiyo chanzo cha dhambi yao.

20 Kwa kuwa walijifanyia utukufu usio na maana kwa njia ya vikuku,wakajifanyia sanamu za miungu zinazochukizapamoja na vitu vyao vya aibu;vyote hivyo nitavifanya kuwa najisi kwao.

21 Utajiri wao nitautia mikononi mwa mataifa mengine,watu waovu wa dunia watauteka na kuutia najisi.

22 Uso wangu nitaugeuzia mbali naoili walitie najisi hekalu langu.Wanyanganyi wataingia humo ndani na kulitia najisi.

23 Tengeneza mnyororo.Kwa kuwa nchi imejaa makosa ya jinai ya umwagaji damuna mji umejaa dhuluma kupindukia,

24 nitayaleta mataifa mabaya sananao watazimiliki nyumba zao. Kiburi chao nitakikomesha,na mahali pao pa ibada patatiwa unajisi.

25 Uchungu mkali utakapowajia,watatafuta amani, lakini haitapatikana.

26 Watapata maafa mfululizo;nazo habari mbaya zitafuatana.Watamwomba nabii maono.Makuhani hawatakuwa na sheria yoyote;na wazee watakosa shauri la kuwapatia.

27 Mfalme ataomboleza,mkuu atakata tamaana watu watatetemeka kwa hofu.Nitawatenda kadiri ya mienendo yao,nitawahukumu kama nilivyowahukumu wengine.Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”