1 Akaniambia, “Wewe mtu, kula unachopewa; kula kitabu hiki kisha uende ukawaeleze Waisraeli.”
2 Kwa hiyo nilifumbua kinywa changu, naye akanilisha hicho kitabu.
3 Halafu akaniambia, “Wewe mtu, kula kitabu hiki ninachokupa, ujaze tumbo lako.” Basi, nilikula kitabu hicho, nacho kikawa kitamu mdomoni kama asali.
4 Kisha akaniambia, “Wewe mtu, waendee Waisraeli, ukawaambie maneno yangu.
5 Sikutumi kwa taifa lenye lugha ngeni na ngumu, bali kwa Waisraeli.
6 Sikutumi kwa mataifa mengi yenye lugha ngeni na ngumu ambayo huifahamu. Kwani ningelikutuma kwa watu kama hao, hakika wao wangekusikiliza.
7 Lakini Waisraeli hawatakusikiliza, kwani hawana nia ya kunisikiliza mimi. Watu wote wa Israeli ni wenye kichwa kigumu na moyo mkaidi.
8 Nimekufanya uwe mgumu dhidi yao, na kichwa chako kitakuwa kigumu dhidi ya vichwa vyao vigumu.
9 Kama almasi ilivyo ngumu kuliko jiwe gumu, ndivyo nilivyokufanya uwe kichwa kigumu. Usiwaogope wala usitishwe na nyuso zao, kwani hao ni watu waasi.”
10 Tena aliniambia, “Wewe mtu, maneno yote nitakayokuambia yatie moyoni mwako, na uyasikilize kwa makini.
11 Kisha nenda kwa watu wako waliopelekwa uhamishoni, ukawaambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi na hivi. Waambie hata kama watakusikiliza au watakataa kukusikiliza.”
12 Kisha roho ya Mungu ikaninyanyua, nami nikasikia nyuma yangu sauti kama ya tetemeko kubwa. “Na usifiwe utukufu wa Mwenyezi-Mungu mbinguni.”
13 Pia nilisikia sauti ya mabawa ya wale viumbe hai yalipokuwa yanagusana, pamoja na sauti ya mgongano wa yale magurudumu kandokando yao.
14 Basi, roho ya Mungu ikaninyanyua juu na kunipeleka mbali. Nikaenda nikiwa na uchungu na ukali rohoni mwangu, nao mkono wa Mwenyezi-Mungu ulikuwa na nguvu juu yangu.
15 Nikawafikia wale watu waliokuwa uhamishoni, waliokuwa wakikaa karibu na mto Kebari huko Tel-abibu. Nikakaa nao kwa muda wa siku saba nikiwa nimepigwa bumbuazi.
16 Baada ya siku saba, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:
17 “Wewe mtu nimekuweka kuwa mlinzi wa Waisraeli. Kila utakaposikia neno kutoka kwangu utawaonya watu kwa niaba yangu.
18 Nikimwambia mtu mwovu kwamba hakika atakufa, nawe humwonyi au kumwambia aache njia yake potovu ili kuyaokoa maisha yake, basi, mtu huyo mwovu atakufa kwa uovu wake; lakini damu yake nitakudai wewe.
19 Lakini, ukimwonya mtu huyo mwovu naye hauachi uovu wake au njia yake potovu, mtu huyo atakufa kwa uovu wake, lakini wewe utakuwa umeyaokoa maisha yako.
20 Tena, kama mtu mwadilifu anauacha uadilifu wake na kutenda uovu, nami nikamwekea kikwazo, mtu huyo atakufa. Kwa vile hukumwonya, atakufa kwa sababu ya dhambi yake, nayo matendo yake ya uadilifu hayatakumbukwa. Lakini damu yake nitakudai wewe.
21 Lakini, ukimwonya mtu mwadilifu asitende dhambi, naye akaacha kutenda dhambi, hakika mtu huyo ataishi, kwa kuwa amepokea maonyo yako, nawe utakuwa umeyaokoa maisha yako.”
22 Nguvu ya Mwenyezi-Mungu ilikuwa juu yangu; naye akaniambia, “Inuka uende mpaka sehemu tambarare nami nitaongea nawe huko.”
23 Basi, nikainuka na kwenda sehemu tambarare. Lo! Nikiwa huko nikauona utukufu wa Mwenyezi-Mungu ukiwa umesimama huko kama utukufu ule niliokuwa nimeuona karibu na mto Kebari; nami nikaanguka kifudifudi.
24 Lakini roho iliniingia na kunisimamisha wima. Kisha Mungu akaongea nami, akaniambia, “Nenda ukajifungie nyumbani mwako.
25 Ewe mtu, utafungwa kwa kamba ili usiweze kutoka na kuwaendea watu.
26 Nitaufanya ulimi wako uwe mzito nawe utakuwa bubu ili usiweze kuwakemea kwa sababu ni waasi.
27 Lakini kila nitakapoongea nawe nitakifungua kinywa chako, nawe utawaambia kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi na hivi, atakayekusikiliza, na akusikilize; atakayekataa kukusikiliza na akatae; maana hao ni watu waasi.