Ezekieli 12 BHN

Nabii kama mkimbizi

1 Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:

2 “Wewe mtu! Wewe unakaa kati ya watu waasi. Wana macho lakini hawaoni; wana masikio lakini hawasikii.

3 Wao ni watu waasi. Basi, ewe mtu, fanya kama vile unakwenda uhamishoni: Ondoka wakiwa wanakuona, ukimbilie mahali pengine. Nenda kama mkimbizi kutoka mahali ulipo mpaka mahali pengine wao wakikuona. Labda wataelewa, ingawa wao ni waasi.

4 Hakikisha wanaona unachofanya. Funga mzigo wako uutoe nje na kuwa tayari kuondoka jioni kama wafanyavyo watu wanaokwenda uhamishoni.

5 Wakiwa wanakuangalia toboa ukuta wa nyumba, upitie hapo na kwenda nje.

6 Wakiwa wanakuona, jitwike mabegani mzigo wako na kuondoka wakati wa giza. Funika uso wako usiweze kuona unakwenda wapi. Ndivyo ninavyokufanya uwe ishara kwa Waisraeli.”

7 Basi, nikafanya kama nilivyoamriwa. Siku hiyo, wakati wa mchana, nikafunga mzigo wangu kama mzigo wa mtu anayekimbia. Jioni nikautoboa ukuta na giza lilipokuwa likiingia, nikatoka, nimejitwika mzigo wangu mabegani, watu wote wakiniona.

8 Kesho yake asubuhi, Mwenyezi-Mungu akaniuliza:

9 “Wewe mtu! Je, hao waasi wa Israeli hawajakuuliza maana ya hicho ulichofanya?

10 Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Kauli hii yangu yahusu mambo yatakayompata mtawala wa Yerusalemu na watu wote wa Israeli wanaoishi humo.

11 Waambie kuwa wewe ni ishara kwao; kama ulivyofanya ndivyo itakavyotendeka kwao: Watakwenda uhamishoni; naam, watachukuliwa mateka.

12 Naye mtawala wao atajitwika mzigo wake mabegani wakati wa usiku, atatoka kupitia ukuta atakaotoboa apate kutoka; atafunika uso wake ili asiione nchi kwa macho yake.

13 Lakini nitatandaza wavu wangu juu yake, naye atanaswa katika mtego wangu. Nitampeleka Babuloni, nchi ya Wakaldayo; naye akiwa huko atakufa bila kuiona hiyo nchi.

14 Wafuasi wake wote, washauri wake na vikosi vyake vyote, nitawatawanya nje kila upande. Nitauchomoa upanga na kuwafuatilia nyuma.

15 Nitakapowatawanya kati ya mataifa mengine na nchi za mbali, ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.

16 Lakini nitawaacha wachache waokoke vitani, wanusurike njaa na maradhi mabaya; ili hao waweze kuwasimulia watu wa mataifa wanamoishi jinsi walivyotenda mabaya. Ndipo watakapotambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

17 Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:

18 “Wewe mtu, kula chakula na kunywa maji yako ukitetemeka kwa hofu.

19 Waambie watu wa nchi hii, kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema juu ya wakazi wa Yerusalemu ambao bado wamo nchini Israeli, kwamba watakula chakula chao kwa hofu na watakunywa maji yao kwa kufadhaika, kwani nchi yao haitakuwa na kitu, kwa sababu kila mkazi ni mdhalimu.

20 Miji yenye watu itateketezwa, na nchi itakuwa ukiwa. Nanyi mtatambua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu.”

Neno la Mwenyezi-Mungu litatimia

21 Neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:

22 “Wewe mtu: Kwa nini methali hii inatajwa katika Israeli: ‘Siku zaja na kupita, lakini maono ya nabii hayatimii?’

23 Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema kwamba nitakomesha methali hiyo nao hawataitumia tena nchini Israeli. Waambie kuwa wakati umewadia ambapo maono yote yatatimia.

24 Maana hapatakuwa tena na maono ya uongo au kupiga bao miongoni mwa Waisraeli.

25 Mimi Mwenyezi-Mungu mwenyewe nitatangaza yatakayotukia. Nayo yatatukia bila kukawia. Wakati wa uhai wenu, enyi watu waasi, neno nitakalotamka nitalitimiza. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.”

26 Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia:

27 “Wewe mtu, Waisraeli wanafikiri kwamba maono yako yanahusu siku za baadaye sana, na unabii wako wahusu nyakati za mbali sana!

28 Kwa hiyo waambie, kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema kuwa maneno yangu yote yatatimia karibuni. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema!”