1 Siku moja baadhi ya wazee wa Israeli walinitembelea kutaka shauri.
2 Basi neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:
3 “Wewe mtu, watu hawa wamekubali mioyo yao itawaliwe na sanamu za miungu; miungu hiyo inawaelekeza kutenda dhambi. Je, nitakubali kuulizwa nao shauri?
4 Basi, sema nao uwaambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema: Mtu yeyote miongoni mwa Waisraeli anayekubali sanamu za miungu zimtawale moyoni, na kuiruhusu miungu hiyo kumwelekeza kutenda dhambi, kisha akaja kumwomba shauri nabii, atapata jibu kutoka kwangu ambalo litazifaa hata sanamu zake nyingi za miungu.
5 Nitaigusa mioyo ya Waisraeli ili wanirudie, kwani wamejitenga mbali nami kwa kuabudu sanamu zao za miungu.
6 “Basi, waambie Waisraeli kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Tubuni, na kuacha kuziabudu sanamu zenu za miungu. Acheni kufanya machukizo.